Rais Shein afungua Kongamano la tatu (3) la Diaspora
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya ufunguzi wa Kongamano la tatu la Watanzania waishio Ughaibuni “Diaspora home coming” lililofunguliwa leo na linatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku mbili katika Hotel ya Zanzibar Beach Resort Visiwani Zanzibar.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo “Bridging Tanzania Tourism and Investment: A new Outlook” MTU KWAO NDIO NGAO ikiwa na lengo la kusisitiza kuunganishwa kwa sekta ya Utalii na Uwekezaji ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya Serikali. Kongamano hili kwa mara ya kwanza linafanyika Zanzibar na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, lilitanguliwa na Makongamano mawili yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Shein katika hotuba yake ya ufunguzi, alieleza jitihada za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kutambua haki na wajibu wa Watanzania waishio Ughaibuni. Hivyo kufuatia umuhimu huo Serikali iliamua kuanzisha Idara ya Diaspora ambayo inasimamia masuala yote ya jumuiya za wanadiaspora popote walipo katika mataifa mengine, sambamba na kuandaa sera ya diaspora ambayo itamtambua mwanadiaspora pamoja na kuainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya utalii na uchumi na namna Wanadiaspora hao wanavyoweza kuchangia katika bajeti ya Serikali kwa kuchangia fedha katika akaunti maalum na katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Vilevile Mheshimiwa Rais Shein akaongeza kwa kusema kuwa “endapo sera hiyo ikikamilika jumuiya za wanadiaspora zitaweza kusoma sera hiyo kupitia Tovuti ya Ikulu na pale itakapohitajika kutunga sheria basi mamlaka zitafanya hivyo”.
Wazizi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye pia alishiriki katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Kongamano, alitumia fursa hiyo kuwaeleza kuwa Tanzania inavivutio vingi na kuwashauri ni vema wakatumia fursa hiyo kuvitangaza vivutio vilivyopo na pia kuvipa kipaumbele vivutio ambavyo bado havijatambuliwa ili viweze kutambuliwa rasmi na kutangazwa duniani kwote na kuiwezesha nchi ya Tanzania kushika nafasi ya juu miongoni mwa mataifa yenye vivutio na maajabu mengi duniani.
Pia alieleza Wizara kupitia Idara ya diaspora inaendelea na utaratibu wa kuandaa mfumo wa kuwatambua wanadiaspora na utekelezaji wake unaelekea kukamilika na kwamba zoezi hilo litakuwa la kuendelea ambapo takwimu zitakuwa zikihuishwa mara kwa mara katika ofisi zote za Ubalozi zinazoiwakilisha nchi ya Tanzania katika mataifa mengine.
Pia aliwaasa wanadiaspora hao kujiepusha kushiriki katika makosa ya kihalifu na makosa mengine ambayo yanapingana na sheria na taratibu za nchi husika. “Wizara yangu wakati mwingine imekuwa ikipokea taarifa za vitendo ambavyo zinaichafua sifa ya nchi yetu au kuleta masikitiko kwa ndugu na jamaa” alisema Waziri Mahiga.
Hivyo ni wakati sasa kila mwanadiaspora akawa balozi wa Tanzania katika nchi anayoishi kwa kutumia vizuri fursa za kimaendeleo zilizopo katika Taifa analoishi, pamoja na kudumisha sifa nzuri ya upendo, amani na mshikamano iliyojengeka tangu siku nyingi, ikiwa ni pamoja na kudumisha utamaduni wa Taifa.
Aidha, Watanzania waishio Ughaibuni walipata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na watoa mada kutoka katika Taasisi na Idara za Serikali pamoja na sekta binafsi zilizolenga katika kuwapa taarifa za taratibu za uwekezaji na miradi mbalimbali inayotekelezwa na mashirika ya Umma na Makampuni binafsi sambamba na kuwaeleza fursa nyingine mpya za miradi ya kiuchumi kama ujenzi, masoko kwaajili ya biashara mbalimbali, utalii pamoja na uwekezaji katika sekta ya viwanda kwa lengo la kuunga mkono sera ya serikali ya awamu ya tano katika adhima yake ya kujenga Tanzania ya viwanda.