Mhe. Membe akipokea Tuzo ya Heshima kwa mchango wake katika kusaidia jamii
Picha na Reginald Philip ================================
Waziri Membe awaasa vijana nchini kumcha Mungu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe amewaasa vijana wa Tanzania kumcha na kumheshimu Mungu kwani wao ndio nguzo ya amani na maendeleo ya nchi.
Waziri Membe ametoa rai hiyo tarehe 05 Aprili, 2015 katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam wakati akihutubia mamia ya watu waliofika uwanjani hapo kuadhimisha miaka 15 ya Tamasha la Pasaka lililoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions.
Mhe. Membe ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha hilo alisema kuwa amani ya nchi inawategemea kwa kiasi kikubwa vijana wenye uadilifu na wanaomcha Mungu, kwani pasipo kufanya hivyo ni rahisi kurubuniwa na kujiunga na makundi mabaya na hatari yakiwemo ya ugaidi.
“Ndugu zangu upo uhusiano kati ya dini, vijana na amani ya nchi. Ni wajibu wa viongozi wa dini zote na Serikali kuhimiza vijana sasa waipende dini kwa sababu ndio msingi wa nchi tunayotaka kuijenga na ni msingi wa uongozi bora na uadilifu ambao utakabidhiwa mikononi mwenu”, alisema Waziri Membe.
Mhe. Membe aliongeza kusema kuwa dini zote duniani zimejikita katika kuleta amani na kusisitiza kuwa vijana wasiende makanisani kwa ajili ya ndoa, misiba na ibada za wagonjwa pekee bali pia waende kwa lengo la kupata mafundisho ya kumcha Mungu kwani taifa lenye vijana wasio waadilifu haliwezi kuwa na viongozi bora.
Awali akimkaribisha Waziri Membe kuzungumza, Askofu David Mwasota wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly alisema kuwa anampongeza na kumshukuru Waziri Membe kwa kuwa tayari wakati wote anapoalikwa kushiriki Tamasha la Pasaka pamoja nao.
“Mhe. Waziri umati huu umefurahishwa sana na uwepo wako. Tunatambua kuwa unazo kazi nyingi za kulitumikia taifa na hata familia yako. Lakini umetambua na kuheshimu umuhimu wa Tamasha la Pasaka na kukubali mwaliko wetu. Ni kwa upendo wako huo katika kushirikiana na watu katika shughuli mbalimbali za kijamii ndio uliokusukuma kuacha mambo mengine yote muhimu na kuja kushirikiana nasi leo, kwa hili tunasema asante sana”, alisema Askofu Mwasota.
Aidha, wakati wa Tamasha hilo tuzo mbalimbalii zilitolewa ikiwemo Tuzo ya Heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua mchango wake katika Sanaa, Tuzo kwa Rais Mstaafu, Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Tuzo ya Heshima kwa Mhe. Membe kwa kutambua mchango wake katika kujishughulisha na shughuli za kijamii na Tuzo kwa Vyombo mbalimbali vya Habari.
Viongozi wengine wa Serikali waliohudhuria Tamasha hilo ni pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Fenella Mukangara, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Angela Kairuki na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Paul Makonda.
Tamasha la Pasaka ambalo lilianzishwa rasmi mwaka 2000 huwashirikisha Waimbaji wa Nyimbo za Injili kutoka nchini na nje ya nchi ambapo Tamasha la mwaka huu limewashirikisha waimbaji kutoka hapa nchini, Afrika Kusini, Uingereza na Zambia.
-Mwisho- |