Matembezi yakiendelea. ==================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Asia na Afrika umemalizika leo hapa jijini Jakarta, Indonesia kwa kushuhudia kupitishwa maazimio muhimu matatu ambayo ni kudumisha ushirikiano miongoni kwa nchi wanachama katika masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na Afrika na Azimio la Palestina.
Mkutano huo pia uliadhimisha miaka 60 ya Ushirikiano baina ya nchi za Asia na Afrika pamoja na miaka 10 ya Mkakati Mpya wa Ubia wa Pamoja kati ya nchi za Asia na Afrika (commemoration of the 60th Anniversary of the Asian-African Conference and the 10th Anniversary of the New Asia-Africa Strategic Partnership).
Lengo la maazimio hayo ni kuongeza ushirikiano zaidi kwa kuzileta pamoja nchi wanachama katika kushughulika changamoto wanazokabiliwa nazo kama vile ukosefu wa amani, ubaguzi wa rangi, matabaka katika jamii, ukosefu wa chakula, ukosefu wa ajira, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, ugaidi, biashara isiyo na usawa, uharamia, ujangili pamoja na mengineyo.
Katika hotuba fupi zilizotolewa na nchi wanachama, nyingi zimeunga mkono suala la taifa la Palestina kupata uhuru wake, kuendelea kushinikiza mageuzi katika Umoja wa Mataifa hususan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Afrika na Asia kwa kuimarisha miundombinu kama vile viwanja vya ndege, njia za mawasiliano, uzalishaji wa nishati ya kutosha, ujenzi wa reli na barabara pamoja kuweka masharti rahisi katika kufanya biashara.
Masuala mengine ni kuachana na utegemezi wa Mashirika ya fedha ya kimataifa ambayo hayana mifumo yenye usawa, kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali, kuongeza ajira na elimu kwa vijana na mengineyo.
Aidha, kwa msukumo sawa na ule unaofanywa na nchi wanachama katika kuisemea Palestina ipate uhuru wake, nchi hizo pia zimeombwa ziweke nguvu sawa na hiyo katika kufanikisha upatikani wa uhuru wa nchi ya Sahara Magharibi.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Asia na Afrika ambapo upande wa Asia alikuwepo Mwenyeji wa Mkutano Rais wa Indonesia, Mfalme wa Jordan, Rais wa China, Rais wa Vietnam, Rais wa Iran, Rais wa Myanmar, Waziri Mkuu wa Japan, Waziri Mkuu wa Thailand, Waziri Mkuu wa Singapore, Waziri Mkuu wa Bangladesh, Waziri Mkuu wa Malaysia na wawakilishi wa viongozi wakuu kutoka mataifa mengine ya Asia katika ngazi ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Mabalozi.
Kwa upande wa Afrika alikuwepo Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mfalme wa Swaziland, Rais wa Madagascar, Rais Siera Leone, Makamu wa Rais wa Afrika ya Kusini na wawakilishi wa viongozi wakuu wa Nchi za Afrika katika ngazi ya Mawaziri na Mabalozi. Tanzania iliwakilishwa na Mhe. Dkt. Mary Nagu (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu na Mahusiano.
Aidha, Wakuu wa Nchi na wawakilishi wa Bara la Asia na Afrika walipata fursa ya kuutembelea mji wa kihistoria wa Bandung ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika. Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Afrika na Asia ulifanyikia katika mji wa Bandung mwaka 1955 ambapo wakuu wa nchi na wawakilishi kutoka nchi 29 zikiwemo nchi saba kutoka Afrika walihudhuria.
Nchi kutoka Afrika zilikuwa ni Algeria, Misri, Ethiopia, Ghana, Liberia, Libya na Sudan ambazo kwa pamoja na zile za Asia walitoka na maazimio kumi katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binadamu kama ambavyo Umoja wa Mataifa unataka, kuheshimu uhuru wan chi na mipaka yake, kutambua usawa wa kimatabaka na nchi, kutoingilia kati masuala ya ndani ya nchi nyingine, kuheshimu haki za kila mtu na mengineyo.
IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM 24 APRILI, 2015
|