MKUTANO NA BI. HENDERSON, MKURUGENZI WA KITENGO CHA AFRIKA MASHARIKI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE YA AUSTRALIA
Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Henderson, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Australia leo tarehe 21 Mei 2015.
Katika mazungumzo yao, waligusia juu ya maendeleo ya maandalizi ya ziara ya Dkt. Kim Hames, Naibu Waziri Mkuu wa Jimbo la Magharibi mwa Australia na Waziri wa Afya na Utalii. Aidha Bi. Henderson aliipongeza Tanzania kwa kuandaa warsha na mikutano ya kutangaza fursa mbalimbali zipatikanazo nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya mafuta, gesi na madini ambapo mwaka jana alihudhuria moja ya warsha iliyofanyika jijini Adelaide, Australia.
Kwa upande wake Balozi Kairuki alichukua fursa hiyo kuishukuru serikali ya Australia kwa nafasi za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na mrefu katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo na Afya.
Kwa kuhitimisha, Balozi Kairuki alimweleza Bi. Henderson juu ya uwepo wa fursa mbalimbali za uwekezaji nchini na kuwasihi wawekezaji kutoka Australia wasisite kuja kuwekeza katika sekta ya madini, nishati na gesi nchini.