Mazungumzo yakiendelea
=================================
TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Tanzania na Algeria zitaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya nchi hizi mbili.
Balozi Mulamula ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Algeria hapa nchini, Mhe. Saad Belabeb ambaye alimtembelea Wizarani leo kwa lengo la kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu.
Katika mazungumzo yao, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania na Algeria zimekuwa na ushirikiano wa karibu na wa kihistoria tangu kipindi cha waasisi wa mataifa haya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais Ahmed Ben Bella na kwamba kuuimarisha ushirikiano huo ni kuendelea kuwaenzi.
Aliongeza kusema kuwa, katika kipindi chote Tanzania na Algeria zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na katika masuala yanayohusu Bara la Afrika chini ya Umoja wa Afrika.
“Tanzania itasimama na Algeria pamoja na marafiki zetu wengine ili kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika na unaendelea mbele zaidi,” alisisitiza Balozi Mulamula.
Kwa upande wake, Balozi Belabeb alimpongeza Balozi Mulamula kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo alimhakikishia ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwake.
Balozi Belabeb alisema kuwa Tanzania ni rafiki muhimu kwa Algeria na hilo linathibitishwa na ziara mbalimbali za viongozi wakuu wa nchi hizi ikiwemo ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete mapema mwaka huu nchini Algeria.
-Mwisho-
|